Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya yasema muafaka na msaada kwa Somalia ni muhimu

Kenya yasema muafaka na msaada kwa Somalia ni muhimu

Makamu wa Rais wa Kenya Kalonzo Musyoka amewataka viongozi wa kisiasa wa serikali ya mpito ya Sonmalia kuafikiana haraka jinsi gani wataisukuma mbele nchi yao ikiwa ni pamoja na kufanya uchaguzi na kuunda taasisi za serikali.

Musyoka aliyekuwa akitoa taarifa mbele ya ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Somalia mjini Nairobi Kenya hii leo , amesema kuna haja ya uongozi wa serikali ya mpito na bunge la nchi hiyo kufanya kazi pamoja ili kupata suluhu ya hatma ya Somalia.

Musyoka ameuambia ujumbe wa baraza la usalama kuwa machafuko ya Somalia ymekuwa yakitia hofu kubwa Kenya tangu kupinduliwa kwa Rais wa zamani wa nchini hiyo Siad Barre mwaka 1991.

Ameitaka jumuiya ya kimataifa kutoa uzito wa hali ya juu kwa masuala ya vita baina ya makundi na koo za Kisomali, wanamgambo na suala la itikadi kali na ameomba msaada wa kibinadamu kwa Somalia uongezwe.

Wajumbe 15 wa baraza la usalama wamekuwa katika ziara maalumu barani Afrika , wakianzia Ethiopia kwa mkutano wa amani na usalama, wamezuru pia Khartoum na Juba Sudan.