Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aipongeza Nigeria kwa huduma za afya ya mama na mtoto

Ban aipongeza Nigeria kwa huduma za afya ya mama na mtoto

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha hatua iliyochukuliwa na serikali ya Nigeria ya kuongeza uwekezaji kwenye sekta zinazohusu afya za wanawake na watoto akisema kuwa Umoja wa Mataifa uko tayari kuupiga jeki mpango huo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea Hospitali ya Maitama iliyopo kwenye mji mkuu wa Abuja, Ban ameeleza kuwa mfumo bora wa afya ambao unawalenga wanawake na watoto ni mfumo ambao umelenga pia jamii nzima.

Amesema kuwa kwa bahati mbaya mifumo mingi ya afya dunia ni ile inayowapuuza wanawake na watoto jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa vifo vingi vya kina mama kutokana na matatizo mbalimbali yatokanayo na hali ya ujauzito mpaka wakati wa kujifungua.

Amehaidi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo ambazo amesema kuwa ni ukombozi mkubwa kwa jamii ya watu wa Nigeria.

Akiwa nchini humo, Ban Ki-moon pia alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Attahiru Jega,na akaipongeza tume hiyo namna ilivyofanikisha uchaguzi mkuu uliopita.