Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika siku ya kimataifa ya bayo-anuai UM wataja faida za misitu

Katika siku ya kimataifa ya bayo-anuai UM wataja faida za misitu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amelezea hofu yake juu ongezeko la ukataji misitu na mmomonyoko wa maeneo ya kilimo cha mbao.

Ban amezitolea wito serikali kutekeleza makubalino ya karibuni ya mkataba wa kimataifa wa kushirikiana rasilimali za urithi wa dunia ikiwemo misitu na mali zitokanazo na misitu hiyo.

Amesema licha ya kutambua na kuthamini mavuno ya misitu lakini yanatoweka kwa kiwango cha kutisha . Ban ameyasema hayo katika ujumbe maalumu wa kuadhimisha siku ya kimataifa ya bayo-anuai ambayo kila mwaka inaadhimishwa Mai 22.

Mwezi Oktoba mwaka jana nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa waliridhia na kupitisha mkataba wa Nagoya , mkataba ambao ni daraja kati ya utunzaji na matumizi endelevu ya bayoanuai kwa ajili ya maendeleo.

Ban amesema kuridhia mapema na kutekeleza mkataba huu kutasaidia kulinda misitu na kuhakikisha matumizi bora ya misitu hiyo kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Ban amesema siku ya kimataifa ya bayo-anuai mwaka huu inakwenda sambamba na mwaka wa kimataifa wa misitu uliopitishwa na baraza kuu la Umoja wa mataifa ili kuelimisha jamii duniani kuhusu thamani,na umuhimu wa kiuchumi, kisiasa na kijamii wa misitu hasa pia katika kuhifadhi mazingira

Amesema katika kulinda misitu, dunia itakuwa inahifadhi mazingira na hivyo kupunguza hatari ya mabadiliko ya hali ya hewa na kupotea kwa bayo-anuai