Skip to main content

WFP imeonya dhidi ya kuzuilliwa misaada ya kibinadamu kwenda magharibi mwa Libya

WFP imeonya dhidi ya kuzuilliwa misaada ya kibinadamu kwenda magharibi mwa Libya

Mkurugenzi mkuu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP Josette Sheeran ameonya kwamba mapigano yanayoendelea yamekuwa kikwazo kikubwa cha kufikia maeneo ya milimani Magharibi mwa Libya ambako mahitaji ya msaada wa chakula ni makubwa.

Bi Sheeran amesema anahofia hali ya kibinadamu na jinsi ya kuweza kuwafikishia chakula maelfu ya watu waliokwama katika eneo hilo kutokana na vita vinavyoendelea.

Ametoa wito kwa pande zote husika katika machafuko kusitisha mapigano mara moja na kuruhusu maeneo hayo kufikika ili mahitaji na msaada wa kibinadamu na hasa chakula uwafifie walengwa.

WFP imepeleka meli mbili mjini Misrata zilizosheheni chakula na misaada mingine kwa niaba ya jumuiya ya kimataifa lakini makombora yanayovurumishwa hivi sasa maeneo ya bandarini yamefanya kuwa vigumu kuingiza msaada.