Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aitaka Libya kuafiki kusitisha mapigano mara moja

Ban aitaka Libya kuafiki kusitisha mapigano mara moja

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameitolea wito serikali ya Libya kuchukua mara moja hatua ya kusitisha mapigano.  Akizungumza mjini Geneva Ban amesema mashambulizi dhidi ya raia ni lazima yasitishwe ili kuruhusu kuingizwa kwa msaada wa kibinadamu.

Ban amesema ni kitu cha kujutia na kusikitisha kwamba madai ya watu ya mabadiliko ya kisiasa na uhuru katika ulimwengu wa Kiarabu yamefikiwa kwa umwagaji damu, ukandamizwaji na ukatili.

Amewataka viongozi kuheshumu haki za binadamu , kuchagiza mazungumzo yatakayojumuisha wote na kuweka mazingira yatakayofuata ushiriki wa wote wa kisiasa na demokrasia.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

Na kuhusu Syria Ban amesema inasikitisha kwamba timu ya tathimini ya masuala ya kibinadamu imezuiliwa kuingia nchini humo licha ya ahadi nyingi za kusema hawatozuiliwa.

Katibu Mkuu amerejea wito wake kwa Rais Assad kwamba asikilize wito wa mabadiliko na uhuru, na kujiepusha kutumia nguvu kupita kiasi kwa watu wanaoandamana kwa amani.