Viongozi wa dunia wawekeze kwenye lishe:WFP

Viongozi wa dunia wawekeze kwenye lishe:WFP

Kuendelea kupanda kwa bei ya chakula duniani kumeacha mamilioni ya familia zikilala njaa, na shirika la mpango wa chakula duniani WFP limetoa wito kwa viongozi wa dunia kuwekeza katika lishe kuepusha hali hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano wan chi masikini duniani unaofanyika mjini Istanbul Uturuki naibu mkurugenzi wa WFP Amir Abdulla amesema watu hawa mara nyingi wanakabiliwa uamuzi mgumu je amlishe nani na amwache nani, adha za huduma za afya na pia kutowapeleka shule watoto wa kike.

Amesema tatizo la utapia mlo ni la kiuchumi kwa nchi masikini na lianaathiri taifa zima. Mwaka huu kupanda kwa bei za chakula, majanga ya asili na machafuko katika sehemu mbalimbali yamewaweka pabaya zaidi watu ambao tayari walikuwa masikini.

Ameongeza kuwa mambo yanabadilika na sasa njaa na utapia mlo umeanza kukumba hata nchi za kipato cha wastani. Mwaka 2010 msaada wa chakula wa WFP ulitolewa kwa watu milioni 100 kwenye nchi zaidi ya 70 zikiwemo 38 ambazo ni masikini sana.

Amesema ingawa juhudi zimeanza kuonekana kupambana na utapia mlo kwa nchi kama Nepal, Mali, Ethiopia, Brazili na Mauritania lakini bado nchi zinatakiwa kuwekeza zaidi katika lishe kuepuka hali hii.