Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano kuhusu michezo katika kuleta amani na maendeleo wango’a nanga Geneva

Mkutano kuhusu michezo katika kuleta amani na maendeleo wango’a nanga Geneva

Awamu ya pili ya mkutano wa kimataifa kuhusu njia ambazo michezo inavyyoweza kuleta amani na maendeleo umengo’a nanga kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Mkutano huo umehudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu kutoka kwa vuguvugu la michezo kwa maendeleo na amani ambapo watazungumzia michezo kama moja ya kichocheo cha kutimiza malengo ya milenia. Kati ya watakaotoa hotuba kwenye mkutano huo ni pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon, rais wa Hungary Pal Schmitt , waziri wa michezo nchini Uingereza Hugh Robertson pamoja na rais wa kamati andalizi ya mashindano ya Rio mwaka 2016 Carlos Nuzman miongoni mwa wengine.

Kwenye hotuba yake ya ufunguzi mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya michezo Wilfried Lemke amesema kuwa ni miaka minne tu imesalia kabla ya kukamilika kwa muda uliowekwa wa kutimizwa kwa malengo ya milenia akisema kuwa jitihada zaidi zinahitajika.