Bosnia na Herzegovina zinakabiliwa na mtafaruku mkubwa kwa hivi sasa:
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo limeambiwa kwamba Bosnia na Herzegovina inakabiliwa na mtafaruku mkubwa tangu kumalizika kwa mapigano 1995, ikiwa bila matumaini ya kuundwa kwa serikali mpya, kudumaa kwa uchumi na tishio la moja kwa moja kutoka Republika Srpska juu ya uwepo wa taifa hilo.
Valentin Inzko mwakilishi wa Boznia na Herzegovina ameliambia baraza la usalama kwamba Republika Srpska moja ya sehemu mbili zinazounda taifa hilo imechukua hatua ambayo inakiuka pakubwa mkataba wa amani ujulikanao kama Dayton Paris Peace Agreement , tangu ulipotiwa saini mkataba huo mwishoni mwa vita 1995.
Mwezi uliopita bunge la Republika Srpska limeamua kufanya kura ya maoni mwezi Juni kuhusu uhalali wa uwezo wa wawakilishi wa ngazi za juu na taasisi nyingi za serikali ikiwemo mahakama ya Bosnia na Herzegovina.
Bwana Inzko amesema endapo hatua hizo zitaruhusiwa kuendelea basi zitakuwa na athari kubwa kwa utendaji na majukumu ya Bosnia na Herzegovina. Makubaliano ya amani yaliafikiwa miaka mine baada ya machafuko ya kikabila na yakaruhusu kuundwa kwa taifa la Bosnia na Herzegovina lililo na pande mbili, Republika Srpska na shirikisho la Bosnia na Herzegovina na kila upande ukiwa na mamlaka yake kamili.