Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wakaribisha muafaka wa kuondoa majeshi Abyei

UM wakaribisha muafaka wa kuondoa majeshi Abyei

Mpango wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa Sudan UNMIS umekaribisha maafikiano ya Sudan Kaskazini na Sudan Kusini ya kuondoa majeshi yao kwenye jimbo la Abyei na kupeleka timu ya pamoja kuweka usalama.

Washiriki katika kamati ya pamoja ya masuala ya kiufundi ya Abyei inayosaidiwa na UNMIS imekubaliana katika mkutano uliofanyika jana Jumapili kuanza kuondoa majeshi yote ambayo hayajaidhinishwa na kupeleka vikosi vya pamoja vinavyojumuisha askari kutoka pande zote kuanzia leo hadi Mai 17.

Pande hizo mbili zimekubaliana kufanya kazi pamoja kuweka mazingira mazuri ya amani, na kuzungumza na jamii za eneo hilo kuhusu kutekeleza mkataba wa amani uliotiwa saini hivi karibuni kwa lengo la kumaliza machafuko jimbo la Abyei.

Machafuko katika jimbo hilo yamekatili maisha ya mamia ya watu na kuwafungisha virago maelfu.