Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana Bulgaria watakiwa kusaidia kukabili changamoto za dunia

Vijana Bulgaria watakiwa kusaidia kukabili changamoto za dunia

Vijana nchini Bulgaria wametakiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kusaidia kukabili changamoto zinazoikabili dunia kama umasikini, mabadiliko ya hali ya hewa na tishio la silaha za nyuklia.

Akihutubia wanafunzi katika chuo kikuu cha Sofia Ban amewaambia kwamba mwezi Oktoba mwaka huu idadi ya watu duniani itafikia bilioni 7 na ifikapo 2050 idadi ya watu itakuwa zaidi ya bilioni 9.

Amesema ni jinsi gani dunia itakuwa miaka 20 ijayo itategemea kwa kiasi kikubwa nini kinafanyika mwaka huu 2011.

Katibu Mkuu amewataka vijana hao kujihusisha na kile alichokielezea kama mambo matatu muhimu yatakayokuwa changamoto kubwa kwa dunia ambayo ni kwanza dunia yenye matarajio mema na kuwa huru na umasikini uliokithiri, pili dunia safi, yenye mazingira bora na endelevu na tatu dunia salama ambayo iko huru bila tishio la silaha za nyuklia.

Amesema kutimiza malengo hayo sio kazi rahisi, na inamaanisha kuwekeza kwa kila hali nguvu na rasilimali.