Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzorota hali ya haki za binadamu Bahrain kunatia hofu:Pillay

Kuzorota hali ya haki za binadamu Bahrain kunatia hofu:Pillay

Hali ya haki za binadamu nchini Bahrain inazidi kuwa mbaya kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa mataifa inayohusika na masuala ya haki za binadamu.

Nchi hiyo imeghubikwa na maandamano ya kupinga serikali ambapo serikali inakabiliana nayo kwa kushikilia mamia ya wanaharakati wa kisiasa na kuwahukumu waandamanaji katika mahakama za siri za kijeshi.

Serikali ya Bahrain inasema watu 400 tuu ndio walioko mahabusu lakini kamishina mkuu wa haki za binadamu Navi Pillay anasema ofisi yake imepokea taarifa kwamba watu wanaoshikiliwa huenda ni zaidi ya 1000.

Wanaoshikiliwa ni pamoja na raia, waalimu, wanasheria, waandishi wa habari, wamiliki wa blog, madaktari, wasanii, wanaharakati na wanachama wa vyombo mbalimbali vya siasa.

Pillay anasema watu wane wakufa mahabusu, wakati madaktari 23 na wauguzi 24 watahukumiwa kwenye mahakama za kijeshi kwa makosa kushiriki maandamano haramu na kuchochea chuki dhidi ya serikali.

Pillay pia ameelezea hofu kuhusu hukumu ya kifo waliyopewa waandamanaji wane wanaodaiwa kuwauwa maafisa wa polisi na ameitaka serikali ya Bahrain kufanya uchunguzi huru kuhusu vifo na pia kuacha kuwatisha na kuwasumbua watetezui wa haki za binadamu na wanaharakati wa kisiasa.