Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia yaungana kukomesha vifo vya ajali za barabarani

Dunia yaungana kukomesha vifo vya ajali za barabarani

 

Tarehe 11 Mai nchi mbalimbali duniani zitaanza kwa mara ya kwanza muongo wa kuchukua hatua kwa ajili ya usalama barabarani 2011-2020. Kuanzia New Zeland hadi Mexico na Urusi hadi Afrika ya Kusini serikali zitajidhatiti kuchukua hatua mpya za kuokoa maisha ya mamilioni ya watu katika barabara zao.

Muongo huo unalengo la kuzuia vifo na majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ambazo wataalamu wanakadiria zitakatili maisha ya watu milioni 1.9 kila mwaka ifikapo 2020.

Shirika la afya duniani WHO linasema watu milioni 1.3 wanakufa kila mwaka na wengine milioni 20 hadi 50 wanajeruhiwa kwa ajali za barabarani wengi wakiwa vijana wa kati ya miaka 15-29.

Muongo huo unaweka mipango maalumu ya hatua zitakazochukuliwa na serikali kukabilia ajali hizo kama anavyofafanua Dr Etienne Krug wa WHO

(SAUTI YA DR ETIENNE KRUG)

Anasema endapo utekelezaji utafanikiwa , mpango huo utashuhudia maisha ya watu milioni 5 yakiokolewa na kuzuia wengine milioni 50 kujeruhiwa katika muongo huo.