Skip to main content

UM waahidi kuendelea kuisaidia Haiti kupambana na kipindupindu baada ya ripoti kutolewa

UM waahidi kuendelea kuisaidia Haiti kupambana na kipindupindu baada ya ripoti kutolewa

Jopo maalumu huru lililoundwa na Umoja wa Mataifa kuchunguza chanzo cha mlipuko wa kipindupindu kilichokatili maisha ya watu zaidi ya 4500 nchini Haiti tangu Oktoba mwaka jana limebaini kwamba mazingira yalichangia na sio kwa sababu ya mtu au kundi fulani.

Ripoti ya jopo hilo la watu wane inayo pia mapendekezo kadhaa kwa Umoja wa Mataifa na serikali ya Haiti ili waweze kusaidia kuzuia mlipuko mwingine na kusambaa kwa haraka ugonjwa huo katika siku za usoni. Jason Nyakundi na taarifa kamili.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon ametangaza kuwa ana mipango ya kubuni jopo kazi kuchunguza matokeo ya ripoti hiyo ili kuhakikisha kuwa hatua mwafaka zimefuatwa.

Karibu watu 300,000 wameambukizwa maradhi ya kipindupindu tangu kuripotiwa kwa ugonjwa huo na hadi sasa watu zaidi wanazidi kuambukizwa huku wengi wakifa.

Wataalamu wanasema kuwa ugonjwa huo haukutokea Haiti kwenyewe bali katoka maeneo mengine barani Asia na kusambaa kwa haraka kupitia mto Artibonite na sehemu zingine nchini Haiti.

Kati ya masuala yaliyochangia kusambaa kwa haraka kwa ugonjwa huo ni pamoja na idadi kubwa ya watu wanaotumia mto huo kwa kuoga, kunywa na starehe zingine na pia idadi kubwa ya watu wanaotumia maji ya mto huo katika kilimo hasa cha mchele.

Pia walioambukizwa walikimbilia vijijini mwao suala lililochangia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huo.