Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa Afrika wajadili kuboresha kilimo:IFAD

Viongozi wa Afrika wajadili kuboresha kilimo:IFAD

Uwezekano wa kilimo kuchangia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo Afrika ndio ajenda kuu katika mkutano wa wakuu wan chi, mawaziri wa kilimo, wataalamu na viongozi wa sekta binafsi wanaokutana leo mjini Cape Town nchini Afrika ya Kusini.

Katika mkutano huo itawasilishwa ripoti ya kimataifa ya ufadhili wa maendeleo ya kilimo na umasikini vijijini kwa mwaka 2011 (IFAD).

Waziri wa kilimo, misitu na uvuvi wa Afrika ya Kusini Tina Joemat-Pattersson, waziri wa kilimo, ushirikiano na usalama wa chakula wa Tanzania Jumanne Abdallah Maghembe wataungana na Rais wa IFAD Kanayo F.Nwanze kutoa mada kuhusu "changamoto mpya, fursa mpya:kilimo Afrika katika karne ya 21".

Ripoti hiyo ya umasikini vijijini mwaka 2011 ambayo ilitolewa Desemba itawasilishwa kwa mara ya kwanza Afrika kwenye mkutano huo ikisisitiza kwamba mabadiliko katika soko la kilimo yanayoa matumaini na fursa mpya hususani Afrika kwa wakulima wadogowadogo, ili kuwasaidia kuinua uzalishaji na hatimaye kukuza uchumi na kupunguza umasikini vijijini.

Ripoti inatoa wito wa kuongezwa ubunifu na uwekezaji ili kuimarisha mazingira ya uchumi kwa kilimo na biashara vijijini jambo ambalo litaboresha maisha ya wakulima wadogo.