Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya Walibya wakimbilia Tunisia:UNHCR

Maelfu ya Walibya wakimbilia Tunisia:UNHCR

Kumekuwa na ongezeko kubwa la wakimbizi wanaohama kutoka katika eneo la milima ya Magharibi mwa Libya na kuingia nchini Tunisia kufuatia kuzuka upya kwa mashambulizi baina ya vikosi vya serikali na vikosi vya waasi wiki iliyopita.

Watu zaidi ya 8,000 wengi wao wakiwa wa kabila la Berbers wameripotiwa kukimbia maeneo yao mwishoni mwa wiki na kuwasili katika eneo la Dehiba,kusin mwa Tunisia. Wengi wa wahamiaji hao ni wanawake na watoto.

Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeonyesha hali ya wasiwasi hasa kutokana na kuharibiwa kwa mahema kadhaa yanayotumika kuhifadhia wakimbizi hao.

Shirika hilo limesema kuwa Walibya wengi hivi sasa wanakimbia maskani zao wakiwa kwenye makundi ya kikabila na huweka kambi za muda kwenye maeneo ya mahema kabla ya kuingia nchini Tunisia.