Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafiri ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo:UM

Usafiri ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo:UM

Viongozi wa kisiasa kote duniani wametakiwa na mkuu wa idara ya uchumi na masuala ya siasa wa Umoja wa Mataifa Sha Zhukang kuhakikisha kunakuwa na uwezekano wa usafiri wa gharama nafuu kwa wote.

Zhukang alikuwa akizungumza kwenye ufunguzi wa mjadala wa wiki mbili ulioanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York ukihusisha tume ya maendeleo endelevu.

Amesema usafiri ni muhimu sana kwa maendeleo, na ni lazima kuhakikisha kunauwezekano wa kuupata tena kwa gharama nafuu hususani kwa watu masikini wanaoishi vijijini, kupanua wigo wa usafiri wa umma na kubadili mfumo wa usafiri ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, uchaguzi wa mazingira na usalama wa nishati .

Mbali ya usafiri tume hiyo pia inaangalia udhibiti wa kemikali, taka na uchimbaji wa madini ili viweze kuwanufaisha watu wahusika. Mada zingine zitakazojadiliwa kwa wiki mbili hizo ni pamoja na haja ya kubadili muundo wa uzalishaji na matumizi ili kushughulikia changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa, mmomonyoko wa mazingira na upungufu wa rasilimali kama maji.