Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo ni muhimu sana katika kuokoa masiha ya mamilioni ya watu duniani:UM

Chanjo ni muhimu sana katika kuokoa masiha ya mamilioni ya watu duniani:UM

Kampeni ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa kutanabaisha umuhimu wa chanjo katika kuokoa maisha hususani ya watoto itamalizika Jumapili wiki hii baada ya wiki nzima iliyoambatana na chanjo, mafunzo, maonesho na mijadala duniani kote.

Wiki ya chanjo mwaka 2011 imeadhimishwa katika nchi 180 katika kanda tano muhimu jambo ambalo limevunja rekodi kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO. Chanjo imetolewa dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo surua, pepo punda, kifaduro, mups, mafua, hepatitis B, polio na homa ya manjano.

Timu ya wataalamu imekuwa ikizuru jamii mbalimbali hasa vijijini ambako huduma za afya ni vigumu kupatikana kutoa chanjo hiyo na kwenye makambi ya wakimbizi wa ndani.

Kwa mara ya kwanza wiki ya chanjo ilifanyika katika nchi za Amerika mwaka 2003 lakini mwaka huu nchi za Afrika na Pacific Magharibi nazo zimeshiriki wiki hiyo kwa mara ya kwanza. Katika ujumbe maalumu wa wiki hii mkuu wa WHO Margaret Chan amesisitiza haja ya kuwa makini dhidi ya maradhi ya kusambaa ambayo yanaweza kuzuilika kwa njia ya chanjo.