Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawasaidia waliokumbwa na mafuriko Namibia

UNICEF yawasaidia waliokumbwa na mafuriko Namibia

Shirika la umoja wa mataifa linalohusika na watoto UNICEF limeendelea na operesheni yake ya utoaji wa huduma za dharura katika eneo la Kaskazini mwa Namibia ambako mamia ya watu wako kwenye hali mbaya kufuatia mvua kubwa iliyosababisha mafuriko yasiyopata kushuhudiwa kwa miaka 120 iliyopita.

Likishirikiana na mashirika mengine ya nchini humo,  UNICEF inasambaza huduma za usamaria mwema ikiwemo lita kadhaa za maji yaliyonyunyizwa dawa maalumu kwa ajili ya kuepusha uwezekano wa kuzuka magonjwa ya mlipuko.

Kulingana na mwakilishi wa UNICEF  nchini humo Ian MacLeod amesema kuwa ni muhimu kwa wakati huu kuhakikisha kwamba usambazaji wa maji safi na salama unazingatiwa ili kuepusha kitisho cha kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.

 

Hatua hiyo inayochukuliwa na UNICEF inalenga kudhibiti kuibuka kwa majanga zaidi ambayo yanadhaniwa kuweza kuibuka. Tayari rais wan chi hiyo Hifikepunye Pohamba ameomba mashirika ya kihisani kutoa msaada wa hali na mali.