Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sera za usalama na afya kazini zizingatiwe:ILO

Sera za usalama na afya kazini zizingatiwe:ILO

Mwaka huu wa 2011 siku ya kimataifa ya usalama na afya kazini inajikita katika kutumia kama nyenzo mifumo ya utawala inayoshughulika na usalama na afya kazini ili kuendelea kuzuia matukio na ajali kazini.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kazi duniani ILO Juan Somavia katika ujumbe maalumu amesema siku hii ambayo huadhimishwa kila mwaka April 28 inakumbusha kwamba kila mwaka watu takribani milioni 37 wanakuwa wahanga wa ajali kazini na zaidi ya milioni 2.3 wanakufa kwa sababu ya majeraha au maradhi yanayohusiana na masuala ya kazi.

Ameongeza kuwa kuanzia kwa wachimba migodi, watalamu wa nyuklia hadi kwenye maofisi ya kawaida ajali na maradhi yanayoambatana na kazi yamesababisha athari kubwa, za vifo na ulemavu zaidi ya magonjwa kama ukimwi na kifua kikuu.

Ameongeza kuwa vifo vingi na majeraha vinatokea bila kuripotiwa na wanaoathrika zaidi ni familia zinazosalia bila ulinzi au msaada wowote na cha kusikitisha zaidi vifo au ajali hizo zingeweza kuzuiliwa kwa kuwa na hatua na mipango maalumu. Katika siku ya leo ILO inasisitiza jukumu la kuwa na mifumo maalumu kuhakikisha usalama na afya kazini.