Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wasomali milioni 2.4 wanahitaji msaada:UM

Wasomali milioni 2.4 wanahitaji msaada:UM

Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban watu milioni 2.4 nchini Somalia wakiwa ni asilimia 32 ya watu wote nchini humo kwa sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu lakini idadi hii huenda ikaongezeka zaidi kutoka na mzozo unaondelea kushuhudiwa nchini humo na ukame wa muda mrefu ambao umesababisha kufariki kwa mifugo wengi.

Kupanda kwa bei ya vyakula na mafuta vimekuwa changamoto kubwa kwa jamii maskini zaidi ambazo pia ziliathirika na ukame wa kati ya mwaka 2007 hadi 2009. Bei ya nafaka inazidi kupanda ikiwa ni kwa asilimia 135 mwezi machi mwaka huu ikinganishwa na wakati kama huo mwaka uliopita.

Mashirika yanayohusika na chakula ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa huenda hali ikawa mbaya zaidi ikiwa ukame utazidi kuwepo na watu kuhama makwao kufuatia mzozo uliopo nchini Somalia.