Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasambaza msaada wa chakula Misrata

WFP yasambaza msaada wa chakula Misrata

Shirika la kimataifa la mpango wa chakula WFP hatimaye limeanza kusambaza huduma ya chakula na mahitaji mengine kwa wananchi wa mji wa Misrata nchini Libya.

Meli yenye vifaa mbalimbali ikiwemo na chakula, madawa, pamoja na magari ya huduma ya kwanza yamewasili kwenye mji huo na tayari wananchi wameanza kusambaziwa huduma muhimu. Hii ni mara ya pili kwa WFP kupeleka meli yake na safari hii zaidi ya watu 23,000 wanatazamiwa kusaidiwa chakula kitachowakimu kwa muda wa mwezi mmoja.

 

WFP inafanya kazi na mashirika mengine ya kimataifa ikiwemo pia chama cha msalaba mwekundi cha Libya ambacho kimepewa jukumu la kusambaza chakula katika maeneo ya Tripoli, Zintan, Yefrin, Nalut, Mezda, Al Reiba na Al Zawia, maeneo ambayo yameathiriwa vibaya na mapigano yanayoendelea.