Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mataifa na serikali 180 zashiriki kampeni ya chanjo ya UM

Mataifa na serikali 180 zashiriki kampeni ya chanjo ya UM

Nchi na mataifa takribani 180 kwa mara ya kwanza yanashiriki kwa pamoja wiki ya kampeni ya chanjo iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa, ikilenga maradhi kama mafua, surua, polio na pepo punda.

Wiki hii ya chanjo iliyoanza siku ya Jumamosi inafanyika katika kanda tano za shirika la afya duniani WHO, ambazo ni Afrika, Amerika ya Kusini, Mashariki mwa Mediteraniani, Ulaya na Pacific Magharibi.

Mkurugenzi wa WHO Margaret Chan amesema ana imani kuwa wiki hii ya chanjo itatoa msisitizo wa haja ya watu kuwa makini na kuzingatia chanjo kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Wataalamu wa afya watakuwa wakizuru jamii mbalimbali hususani za vijijini kutoa chanjo hiyo, pia kutatolewa mafunzo maalumu na warsha kwa wahudumu wa afya, itakayoambatana na mijadala kutoka kwa wanaotoa maamuzi, wataalamu, wagonjwa na watoa huduma.