Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhalifu wa vita umetekelezwa na serikali na waasi Sri Lanka

Uhalifu wa vita umetekelezwa na serikali na waasi Sri Lanka

Jopo maalumu la wataalamu wa kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kuhusu masuala muhimu kwenye mgogoro wa Sri Lanka wamebaini ripoti za uhalifu wa kivita uliotekelezwa na serikali na waasi wa Tamil Tigers.

Katika ripoti maalumu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa jopo hilo pia limetoa wito wa kufanyika uchunguzi wa kina dhidi ya madai hayo. Uamuzi wa kutoa ripoti hiyo hadharani baada ya kukabidhiwa kwa Katibu Mkuu April 12 na kwa serikali ya Sri Lanka, umefanywa kwa kuzingatia masuala ya uwazi na matakwa ya umma.

Ban anatumai kwamba ripoti hiyo ya ushauri itasaidia kuhakikisha uwajibikaji na haki ili serikali na watu wa Sri Lanka waweze kusonga mbele kuelekea maridhiano na amani ya kudumu.

Ban amesema anapitia kwa makini hitimisho na mapendekezo ya ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na tathimini ya madai ya ukiukwaji mkubwa wa sheria na haki za kimataifa kwa serikali na waasi, madaia mbayo mengine yanaweza kuwa ni uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kama kuuwa raia na kuzuia kupata msaada wa kibinadamu.

Vita vilimalizika May 2009 ambapo majeshi ya serikali yalijitangazia ushidi dhidi ya waasi wa Tamili Tigers baada ya miongo mitatu ya machafuko. Maelfu ya watu walipoteza maisha na mamilioni kuwa wakimbizi wa ndani.