Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya utulivu yarejea mji wa Abidjan

Hali ya utulivu yarejea mji wa Abidjan

Hali inaripotiwa kuwa tulivu kwenye mji mkuu wa Ivory Coast Abidjan baada ya kutokea kwa mapigano Alhamisi iliyopita.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast UNOCI wamekuwa wakipiga doria mjini humo baada ya wanajeshi waaminifu kwa rais wa zamani Laurent Gbagbo kuwashambulia wanajeshi wa rais Alassane Ouattara. Gbagbo alisalimu amri kwa rais Ouattara baada ya mvutano wa kisiasa iliodumu kwa muda wa miezi minne ambapo alikataa kuondoka madarakani . Hamadoun Toure ni msemaji wa UNOCI

"Hatuna fursa nyingine ya kukutana naye. Yuko chini ya kizuizi cha serikali. Tumeona dalili za matumani katika mapatano. Spika wa bunge amekutana na rais Ouattara. Tunatarajia kuwa ataapishwa hivi karibuni na ninaweza kusema kwa njia ya kawaida. Mnavyojua hakuapishwa rasmi."

Mjini Abidjan maelfu ya watu wamehama makwao ili kutafuta maeneo salama wakati ambapo zaidi ya watu 100,000 wanapokadiriwa kuhama makwao katika maeneo ya magharibi.