Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya Misrata:OCHA

Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya Misrata:OCHA

Juhudi za misaada zitaongezwa ili kukabiliana na hali mbaya ya kibinadamu mjini Misrata Libya umesema Umoja wa Mataifa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA imesema itaongeza uwepo wake kwenye mji mkuu Libya ili kuweza kutoa msaada kwa maelfu ya watu waliojikuta katikati ya mapigano mjini Misrata.

Afisa wa OCHA nchini Misri Zlatan Milisic anasema bado ni vigumu kuapta taarifa kamili ya nini kinachotokea Misrata kwani si rahisi kwenda huko kutokana na mapigano yanayoendelea na hali inazidi kuwa mbaya kila siku.

Wakati huohuo OCHA inasema watu takriban 8000 wengi wakiwa wahamiaji kutoka Afrika na Asia wameshahamishwa kutoka mjini Misrata, na meli nyingine inatazamiwa kuwasili Misrata hii leo kupeleka tani 160 za chakula, madawa, mahema na magodoro kwa watu waliokwama, pia itaondoka na wahamiaji wengine kuwapeleka Benghazi.