Matatizo ya nyumba ni makubwa Argentina:Rolnik

Matatizo ya nyumba ni makubwa Argentina:Rolnik

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya nyumba Raquel Rolnik amesema anatiwa hofu na vitendo vya kuhamisha watu kwa nguvu na upungufu wa nyumba bora katika maeneo mengi nchini Argentina.

Bi Rolnik ambaye amehitimisha ziara yake nchini humo amesema licha ya serikali kufanya maamuzi muhimu 2003 ya kuhakikisha masuala ya nyumba ni jukumu la serikali , haijatekeleza ahadi hiyo. Amesema wakulima, watu wa asili wanaoishi katika makazi yasiyo rasmi wanahamishwa kwa nguvu bila kupewa suluhisho. Jason Nyakundi anaarifu.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Bi Rolnik amesema kuwa kwa vile hakujakuwa na nyumba wanazoweza kugharamia wenyeji hali hii imechangia kuwepo kwa unyakuzi wa ardhi kama moja ya njia ya kujipatia makao nchini Argentina .

Hali hii imesababisha watu wanaonyakua ardhi na nyumba katika maeneo mengine kuonekana kama wahuni. Anesema kuwa ameshuhudia misongamano mikubwa kutokana na kuwepo ukosefu wa ardhi na nyumba nafua wanazoweza kukidhi waishio mijini.

Rolnik anaongeza kuwa hata baada ya serikali kuanza kutenga fedha tangu mwaka 2003 kutatua tatizo la uhaba wa nyumba bado suluhu haijapatikana. Amesema kuwa tatizo la uhaba wa makao na ardhi limeendelea kushuhudiwa baada ya Argentina kushuhudia ukuaji wa uchumi ambao umechangia kuongezeka kwa bei ya ardhi na kodi za nyumba.