Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Malaria, UM unataka juhudi zaidi kudhibiti ugonjwa huo

Siku ya Malaria, UM unataka juhudi zaidi kudhibiti ugonjwa huo

Siku ya Malaria duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka ni ya kutathimini juhudi zilizopigwa kimataifa katika kudhibiti ugonjwa huo unaouwa mamilioni ya watu duniani limesema shirika la afya duniani WHO.

Siku hiyo ni Aprili 25 na mwaka huu inaambatana na kauli mbiu "kupiga hatua na mafanikio kunahitaji juhudi mpya za kimataifa ili kufikia lengo la vifo sufuri vya malaria ifikapo 2015". Katika ujumbe maalumu wa siku hiyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema Siku ya Malaria inatoa fursa kwa wote kuleta mabadiliko, iwe serikali, kampuni, shirika la hisani au mtu binafsi, unaweza kukomesha malaria na kusaidia kuinua afya na maendeleo ya jamii.

WHO inasema kupunguza athari za malaria ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia yaliyoafikiwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Shirika hilo limesema wadau mbalimbali zikiwemo serikali, mashirika ya kimataifa, makampuni, wanazuoni, taasisi za utafiti, mifuko ya hisani, NGO's na watu binafsi wameanza kupiga hatua katika vita dhidi ya malaria na wataendelea kutanabaisha changamoto zilizosalia kufikia malengo.

Mwaka 2009 watu takribani bilioni 3.3 nusu ya watu wote duniani walikuwa katika hatari ya kupata malaria, na kila mwaka watu milioni 250 wanaugua ugonjwa huo na 800,000 hufariki dunia wengi wakiwa kutoka nchi masikini hasa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Dr Awa Marie Coll-Seck ni mkurugenzi mtendaji wa mpango wa kupunguza malaria, Roll Back Malaria Partnership anasema kiasi hatua zimepigwa kudhibiti ugonjwa huo.

(SAUTI YA DR AWA MARIE COLL-SECK)