Kuna matatizo makubwa ya kisaikolojia katika shule Gaza:UNESCO

Kuna matatizo makubwa ya kisaikolojia katika shule Gaza:UNESCO

Matatizo ya kuwa na woga, huzuni, hofu ya kushambuliwa, kushindwa kutulia darasani na matokeo mabaya ya mitihani ni baadhi ya matatizo yanayowakabili wanafunzi na waalimu kwenye Ukanda wa Gaza eneo la Wapalestina linalokaliwa.

Hii ni kwa mukibu wa tathimini ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO ambayo inainyesha mfumo wa elimu unaathirika vibaya kutokana na operesheni za kijeshi za karibuni na vikwazo vinavyoendelea Gaza.

UNESCO inasema karibu asilimia 83 ya wanafunzi wamearifiwa kuwa na wasiwasi, asilimia 57, wanahofia maisha yao shuleni, asilimia 67 wanahisi hawana usalama wanapokwenda na kurudi toka shule na zaidi ya asilimia 70 wanapata majinamizi na kuhofia kuzuka kwa vita vingine.

Matokeo katika elimu pia yameathirika huku asilimia 77ya waalimu wa shule za awali, msingi na sekondari wakiarifu alama za chini kwa wanafunzi wao mara kwa mara au wakati wote. Na theluthi mbili ya wanafunzi wa chuo kikuu waliohojia wanahisi kuwa na matumaini madogo sana ya maisha yao ya baadaye.

Nao waalimu waliohojiwa theluthi mbili wamesema wanasumbuliwa na msongo wa mawazo na ugumu wa kudhibiti nidhamu ya wanafunzi darasani. Ripoti hii imekuja wakati ikiandaliwa ripoti ya kimataifa ya masuala ya elimu kwa 2011 ambayo kauli mbiu yake mwaka huu ni "Elimu na machafuko ya vita".