Mfanyakazi wa UM UN-HABITAT apata tuzo ya kimataifa ya Magnum ya upigaji picha
Mfanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT Julius Mwelu ametunukiwa tuzo yenye hadhi kubwa iitwayo Magnum Foundation Emergency Fund Award kutokana na kazi yake ya upigaji picha.
Mfuko wa Magnum umekuwa ukiwasaidia wapiga picha wenye uzoefu ambao wanafanya kazi ya tanabaisha masuala muhimu ambayo mara nyingi hayaripotiwi au kupewa uzito na vyombo vya habari.
Wataalamu 10 wa masuala ya upigaji picha walichagua wapiga picha 100 kutoka kila pembe ya dunia kuwasilisha mapendekezo yao ya picha za matukio hayo na walichaguliwa kutokana na uzito wa kazi yao na umuhimu wa masuala waliyoyapendekeza kushughulikia .
Miongoni mwa majaji ni mkurugenzi wa masuala ya picha wa Magnum ambaye pia ni profesa wa chuo kikuu cha Suffolk, waandishi maarufu wa vitabu Philip Gourevitch na Marc Kusnez na pia mtayarishaji wa zamani wa shirika la habari la NBC, na mtetezi wa haki za binadamu.
Kati ya wapiga puicha hao 100 Julius Mwelu kutoka Afrika Mashariki nchini Kenya anayefanya kazi na UN-HABITAT ndio akajitwalia tuzo hiyo jambo ambalo limekuwa fahari kubwa sio kwake peke yake bali pia kwa shirika la UN-HABITAT.
Je ni picha za aina gani, zinazoelezea matukio gani zlizomfanya kuibuka kidedea dunia nzima? Na tuzo aliyopata inamsaidia vipi yeye na jamii yake? Mwandishi wetu mjini Nairobi Jason Nyakundi amekwenda kukutana naye, ungana nao katika makala hii .