Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siasa zitakazojumuisha wote zinahitajika Libya:Ban

Siasa zitakazojumuisha wote zinahitajika Libya:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anayehudhuria mkutano wa pande tano kuhusu Libya mjini Cairo Misri amesema Umoja wa Mataifa unatiwa hofu kutokana na kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini Libya.

Amesema kwa mujibu wa shirika la kimataifa la uhamiaji IOM na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR takriban watu nusu milioni wamekimbia Libya tangu kuzuka machafuko mwezi uliopita, huku wengi wakikwama kwenye makambi na vituo vya muda kwenye nchi jirani.

Ameongeza kuwa suala lingine linatowatia hofu ni raia wan chi ya tatu yaani wafanyakazi wahamiaji na wakimbizi waliojikuta wamekwama kwenye mapigano yanayoendelea nchini humo. Katika hotuba yake amesisitiza kwamba Umoja wa mataifa unajihusisha na mchakato wa mipango maalumu ya kuwasaidia watu wa Libya kujenga mustakhbali wa maisha yao.

(SAUTI YA BAN KI-MOON)