Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi 12 wa misaada waachiliwa huru Darfur

Wafanyakazi 12 wa misaada waachiliwa huru Darfur

Wafanyakazi 12 wa misaada waliokuwa wanashikiliwa mateka na kundi moja ndani ya kambi ya wakimbizi wa ndani ya Kalma Kusini mwa Darfur wameachiliwa.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq wafanyakazi hao ambao ni Wasudan wameachiliwa kwa msaada wa mpango wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika UNAMID. Haq amesema wafanyakazi hao walishikiliwa mateka siku ya Jumatatu kufuatia maafisa wa usalama kumkamata mkazi mmoja wa kambi hiyo siku mbili kabla.

Utekaji huo umesababisha makundi ya wafanyakazi wa misaada kusitisha kazi zao ndani ya kambi ya Kalma lakini wanatarajiwa kuanza kupeleka tena misaada hivi karibuni. Wakati huohuo UNAMID inasema inachunguza ripoti ya mapigano ya karibuni baina ya jeshi la Sudan na makundi ya waasi.