Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama lapitisha azimio kukabili uharamia Somalia

Baraza la usalama lapitisha azimio kukabili uharamia Somalia

Kwa kutambua haja ya hatua zaidi za kupambana uharamia, leo baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kufikiria hatua za haraka za kuanzisha mahakama maalumu Somalia za kuwafungulia mashitaka na kuwahukumu maharamia Somalia na ukanda mzima.

Baraza pia limezitaka nchi na wadau mbalimbali wanaoathirika na uharamia hususani jumuiya ya kimataifa ya safari za meli kutoa msaada kwa mfuko maalumu ulioanzishwa kushughulikia kuanzishwa kwa mfumo wa sheria, mahakama na miradi ya kupambana na uharamia.

Wajumbe wote 15 wa baraza la usalama wamepitisha bila kupingwa azimio linalosisitiza haja ya mkakati madhubuti wa kimataifa wa kukabiliana na uharamia na sababu zake na kutaja baadhi ya hatua muhimu za kuchukuliwa.

Hatua hizo ni pamoja na kuyataka mataifa yote kushirikiana katika suala l kuchukua mateka, kuyachagiza mataifa na mashirika ya kiknda kuisaidia Somalia kuimarisha ulinzi wake katika pwani ya bahari ya Hindi, kuyataka mataifa yote yakiwemo ya kanda ya pembe ya Afrika kuufanya uharamia kuwa kosa la jinai katika sheria zake na kusistiza haja ya kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wanaofadhili uharamia, kupanga, au kufaidika na mashambulizi ya maharamia kwenye pwani ya Somalia.