Skip to main content

Ban kuongoza mkutano kuhusu Libya wiki hii

Ban kuongoza mkutano kuhusu Libya wiki hii

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatarajiwa kusafiri kwenda nchini Misri juma hili ambapo ataongoza mkutano ulioitishwa wenye lengo la kuhakikisha kuwa jamii ya kimataifa inaendelea kushughulikia hali iliyopo kwa sasa nchini Libya.

Kulingana na msemaji wake mkutano huo utaandaliwa kwenya makao makuu ya muungano wa nchi za kiarabu mjini Cairo ambapo kati ya watakaohudhuria watakuwa miongoni mwao Katibu Mkuu wa muungano wa nchi za kiarabu Amre Moussa, mwenyekiki wa tume ya muungano wa Afrika Jean Ping pamoja na mwakilishi wa muungano wa Ulaya katika masuala ya kigeni Catherine Ashton.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwenye mkutano huo utawajumuisha waakilishi kutoka shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa pamoja na kutoka shirika la kuratibu masuala ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA. Kulingana na OCHA zaidi ya tani 600 za chakula kinachoweza kuwalisha watu 4,000 kwa mwezi mmoja kiko njiani na kitasambazwa katika siku zijazo.