Machafuko Misrata lazima yasite mara moja:UNICEF

11 Aprili 2011

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF leo limetoa wito wa kusitishwa mara moja mashambulizi kwenye mji wa Misrata Libya likionya kwamba maelfu ya watoto wako katika hatari kubwa.

UNICEF inasema kushika kasi kwa mapigano na mashambulizi kumeongeza idadi ya watoto waliouawa kwenye machafuko hayo mjini Misrata, huku wengine wengi wakikosa chakula, maji safi, na kuathirika kisaikolojia kutokana na kushuhudia mashambulizi na mauaji. Jason Nyakundi anaripoti.

(SAUTI YA JASON NYAKUNDI)

UNICEF inasema kuwa imethibitisha madai kuwa watoto hata walio na umri wa miezi tisa wameuawa kwenye mji wa Misrata na wengi kujeruhiwa kutokana na majeraha ya risasi na mashambulizi ya maguruneti. Vifo hivi vimetokea kwa muda wa siku 20 zilizopita huku wengi wa waathiriwa wakiwa na umri wa chini ya miaka kumi.

Mkurugenzi wa shirika la UNICEF katika eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika Shahida Azfar anasema kuwa watoto wengi zaidi wanaendelea kuuawa , kujeruhiwa na kunyimwa mahitaji yao kufuatia mapigano yanayoshuhudiwa.

Huku mapigano ndani na nje ya mji wa Misrata yakiingia wiki yake ya saba na maelfu ya watoto wakijipata kati kati mwa mapigano hayo, UNICEF imerejelea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon wa kuzitaka pande husika kusitisha mapigano

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter