Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Laurent Gbagbo asalimu amri, sasa yuko chini ya ulinzi

Laurent Gbagbo asalimu amri, sasa yuko chini ya ulinzi

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Ivory Coast UNOCI umethibitisha kwamba kiongozi wa nchi hiyo aliyegoma kuondoka madarakani Laurent Gbagbo amekamatwa na majeshi ya mpinzani wake Alassane Ouattara.

Gbagbo na mkewe wamekabidhiwa kwenye hotel ya Golf ambayo ni makao makuu ya Ouattara baada ya kutolewa kwenye handaki lililoko kwenye kasri lake kwa msaada wa wanajeshi wa Ufaransa mjini Abidjan.

Afisa wa UNOCI Hamadoun Toure anasema hivi sasa Umoja wa Mataifa uko tayari kwa msaada utakaohitajika kwa bwana Gbagbo unatoa ulinzi kwa mujibu wa jukumu la baraza la usalama.

(SAUTI YA HAMADOUN TOURE)

Naye balozi wa Ivory Coast kwenye Umoja wa Mataifa ambaye aliteuliwa na Alassane Ouattara Youssef Bamba ametoa hisia zake kuhusu kukamatwa huko kwa Laurent Gbagbo

(SAUTI YA YOUSSEF BAMBA)

Kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York baraza la usalama limekutana kwa dharura kujadili suala hilo la Ivory Coast na kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa operesheni za kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Alain Le Roy.

Bwana Gbagbo alikataa kuondoka madarakani baada ya kushindwa kwenye uchaguzi mkuu mwezi Novemba mwaka jana ambapo mpinzani wake Alassane Ouattara alitangazwa mshindi na tume ya uchaguzi na kutambulika kimataifa suala lililozua machafuko makubwa. Watu zaidi ya 1000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni kuwa wakimbizi.