Skip to main content

Mawaziri wa Afrika waafikia mkataba wa magonjwa yasiyoambukiza

Mawaziri wa Afrika waafikia mkataba wa magonjwa yasiyoambukiza

Mkutano wa mawaziri wa afya kuhusu magonjwa yasiyoambikiza umekamilika nchini Congo ambapo uamuzi wa kutekelezwa kwa makubaliano ya Brazaville uliafikiwa.

Makubaliano hayo yanatoa wito kwa hatua za dharua kuchukuliwa na washika dau ili kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika. Miongoni mwa magonjwa haya ni ugonjwa wa kisukari, Ugonjwa wa saratani, magonjwa ya damu pamoja na ya akili. George Njogopa anaripoti.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Azimo hilo la mawaziri wa afya linatilia uzito juu ya kuimarishwa na kuweka uwiano sahihi wa mifumo ya afya katika ngazi ya taifa na wakati huo huo kuhakikisha kwamba elimu ya uelewa kwa wananchi inatolewa kuhusiana na magonjwa hayo.

Kuwepo kwa mipango endelevu ya kudhibiti, kuzuia na kuchanganua hali jumla ya mambo kwa shabaya ya kuiepusha jamii kutoangukia kwenye magonjwa hayo ni maeneo mengine yanayopewa kipaumbele na tamko hilo ambalo pia limezingatia maeneo mengine kama suala la matumizi ya kupindukia ya pombe, kukosekana kwa lishe bora na uvutaji wa sigara.

Mawaziri hao wa afya wameahaidi kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi ili kutoa matunda mema juu ya azimio hilo na wakawataka wakuu wa nchi na serikali zao kuidhinisha azimio hilo na kisha kulifikisha kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika septemba mwaka huu 2011.