Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa wiki ijayo ni muhimu sana kwa Wasomali:Mahiga

Mkutano wa wiki ijayo ni muhimu sana kwa Wasomali:Mahiga

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Balozi Augustine Mahiga leo amesema mkutano wa ngazi ya juu wa majadiliano uliopangwa kufanyika wiki ijayo mjini Nairobi Kenya ni muhimu sana kwa Wasomali.

Mahiga amesema mkutano huo wa tarehe 12 na 13 April utafanyika kama ulivyopangwa na amepokea majibu mazuri kutoka katika pande mbalimbali na maafisa wa serikali ya mpito ya Somalia walio tayari kushiriki kwa lengo la kuimarisha mazungumzo baina ya serikali ya mpito na washirika wake. Jason Nyakundi ana ripoti.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Balozi mahiga anasema anaamini kuwa makundi madogo ambayo yanapinga kufanyika kwa mkutano hayaelewi lengo kuu la mkutano huo. Mahiga anasema kuwa wajibu wa Umoja wa Mataifa ni kusaidia akiongeza kuwa visa vya hivi majuzi vinaonyesha kuwa kumekuwa na mvurugano wa majadilionio kati ya serikali ya mpito na washirika wake.

Mahiga ameongeza kuwa mkutano huu utatoa mwelekeo wa kufanyika kwa mkutano mwingine mjini Mogadishu kulingana na mapendekezo ya serikali ya mpito. Balozi Mahiga amesema kuwa mkutano huu utalenga zaidi majukumu yanayostahili kutekelezwa ili kumaliza muda wa serikali ya mpito kwa njia inayowanufaisha wasomali.

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa pamoja na jamii ya kimataifa wako tayari kusaidia kuwepo kwa majadiliano na katika kuisadia serikali ya mpito na Wasomali.