Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bei za chakula zimeanza kupungua duniani:FAO

Bei za chakula zimeanza kupungua duniani:FAO

Bei za kimataifa za chakula zimepungua kidogo katika mwezi Machi na kusitika mzunguko wa takribani miezi minane wa kupanda kwa gharama za chakula limesema leo shirika la chakula na kilimo FAO.

Kwa wastani bei ya bidhaa muhimu kama mafuta, sukari na nafaka imepungua kwa asilimia tatu. FAO inasema hata hivyo kupungua huko ni kwa kiasi kidogo na kwa ujumla bei za chakula bado ziko juu. David Hallam kutoka FAO anasema kupungua huko ni faraja lakini itakuwa mapema mno kusheherekea na kuona haya ni mapinduzi ya gharama za chakula.

Ameongeza kuwa katika mwezi wa Machi bei za nafaka duniani zilipungua kwa asilimia 2.6 wakati bei ya mafuta ikienda chini kwa asilimia 7 huku bei ya sukari ikiporomoka kwa asilimia 10.