Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Washukiwa wa machafuko ya uchaguzi Kenya wapanda ICC

Washukiwa wa machafuko ya uchaguzi Kenya wapanda ICC

Wakenya watatu wanaoshutumiwa kuchagiza machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu nchini Kenya mwaka 2008 wamepanda kizimbani kwa mara ya kwanza kwenye mahakama kuu ya kimataifa ya uhalifu ya ICC iliyoko The Hague .

Wanasiasa sita ambao pia walikuwa maafisa wa serikali waliitwa katika mahakama ya ICC wakihusishwa na ghasia za baada ya uchaguzi. Wa kwanza kufika mbele ya mahakama hii leo ni waziri aliyesitishwa kazi William Ruto na Henry Kosgey na pia mwandishi habari Joshua Arap Sang.

Washukiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwemo mauaji, kuwahamisha watu kwa nguvu na utesaji. Wakati wa kusomewa mashitaka yao jaji aliwataka wote watatu kujitambulisha na kuwauliza endapo wamefahamishwa ipasavyo kuhusu madai yanayowakabili na haki zao.

Madai ya udanganyifu katika uchaguzi wa Rais wa Desemba 2007 yalichochea kuzuka kwa machafuko yaliyosababisha watu zaidi ya 1500 kuuawa na wengine zaidi ya 300,000 kuwa wakimbizi wa ndani. Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Luis Moreno Ocampo anawasilisha kesi mbili katika mahakama hiyo ambazo zinawshutumu wapinzani na maafisa wa serikali kwa kuchochea ghasia.

Kesho Ijumaa aliyekuwa waziri wa fedha Uhuru Kenyatta, katibu wa bunge Francis Muthaura na mkuu wa zamani wa polisi Hussein Ali watafika mbele ya mahakama kusikia mashitaka yao ya mauaji, kuhamisha watu kwa nguvu, ubakaji na utesaji.