Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haiti itaendelea kuhitaji msaada wa kimataifa Ban aliambia baraza la usalama

Haiti itaendelea kuhitaji msaada wa kimataifa Ban aliambia baraza la usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ameahidi kuendelea kutoa msaada wa Umoja wa Mataifa kwa nchi ya Haiti.

Amesema nchi hiyo ingawa imepiga hatua kubwa katika miezi ya karibuni lakini bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kufufua uchumi na kuimarisha utawala wa sheria.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza la usalama kinachojadili Haiti hii leo Ban amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa bega kwa began a na serikali na watu wa Haiti kwa masuala yote muhimu ikiwemo ujenzi mpya na hatma ya baadaye ya taifa hilo.

Kikao hicho cha baraza la usalama kimeitishwa na Colombia ambayo ndio rais wa mzunguko wa baraza kwa mwezi huu wa Aprili. Kikao hicho kinafanyika wakati Haiti na washirika wa kimataifa wanatathimini hatua zilizopigwa kufuatia uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali mwanamuziki nyota Michel Martelly amemshinda mke wa zamani wa Rais bi Mirlande Manigat katika uchuguzi huo wa Rais.

Ban amewapongeza watu wa Haiti kwa hatua hiyo muhimu ya kuelekea demokrasia na kuongeza kwamba taifa hilo la Caribbean limepiga hatua kwa msaada mkubwa wa mpango wa Umoja wa Mataifa kulinda amani nchini Haiti MINUSTAH, hasa katika usalama, kuheshimu uhuru na haki za binadamu na kumaliza ghasia na amempongeza Rais anayemaliza muda wake Rene Preval ambaye pia ameshiriki kikao cha leo cha baraza la usalama.