Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN-HABITAT kufanya mkutano kujadili mipangilio ya miji

UN-HABITAT kufanya mkutano kujadili mipangilio ya miji

Wajumbe kutoka sehemu mbali mbali duniani wanatarajiwa kukutana mjini Nairobi nchini Kenya kwenye mkutano wa baraza la shirika la makaazi la Umoja wa Mataifa la UN-HABITAT unaotarajiwa kung\'oa nanga tarehe 11 na kumalizika tarehe 15 mwezi huu.

Baraza hilo kawaida huwa linakutana baada ya miaka miwili kujadili huduma za shirika la UN-HABITAT na uhusiano katika yake na washirika wake. Wakati wa mkutano huo mkurugenzi mpya wa shirika hilo Joan Clos ambaye awali alikuwa Meya wa mji wa Barcelona atatoa mipango yake na kuelezea ajenda ya shirika hilo kwa miaka inayokuja.

Mkutano huo wa juma moja utahudhuriwa na mawaziri , maafisa wa ngazi za juu na waakilishi wengine wa serikali wakiwemo washirika wa shirika la UN-HABITAT ambapo pia suala la athari za mabadiliko ya hali ya hewa mijini litajadiliwa.