Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataka jumuiya ya kimataifa kutosahau mgogoro wa Somalia

UNHCR yataka jumuiya ya kimataifa kutosahau mgogoro wa Somalia

Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Antonio Guterres amesema mgogoro wa Somalia unaweza kufikia kiwango cha kutopata suluhu endapo jumuiya ya kimataifa haitoongeza mara mbili jitihada za kutatua mgogoro huo.

Guterres amesema sasa dunia imejielekeza kwa yanayotokea Japan, Ivory Coast, Libya na nchi zingine Mashariki ya Kati, ametoa wito wa kutoisahau Somalia, amesema kwa kufanya hivyo gharama zake zitakuwa kubwa, kwani vita vilivyoanza Somalia miaka 20 iliyopita bado vinaendelea. Jason Nyakundi ana taarifa zaidi.

(RIPOTI YA JASON NYAKUNDI)

Guterres amesema kuwa mshikamano wa kimataifa una umuhimu mkubwa katika kuendelea kutatua shida zinazoikumba Somalia na wasomali. Amesema kuwa watu 700,000 kati ya watu milioni 1.5 waliokimbia makwao kutokana na mapigano yaliyodumu kwa miongo miwili, wanaishi kwenye makambi sehemu mbali mbali duniani huku Kenya ikiwapa hifadhi wakimbizi 330,000.

Guterres amesema kuwa kwa sasa wakimbizi 10,000 kutoka Somalia wanavuka mpaka na kuingia Kenya kila mwezi akiongeza kuwa hili ni tatizo linalohitaji jitihada zaidi kulitatua. Guterres amesema kuwa shirika lake linakamilisha mazunguzmo na serikali ya Kenya kuhusu masuala haya likiwemo suala la kuiomba serikali ya Kenya kuwapa ulinzi wakimbizi hao.