Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC huenda ikachunguza mauaji Ivory Coast

ICC huenda ikachunguza mauaji Ivory Coast

Ofisi ya mwendesha mashitaka wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC imesema inahofia kuendelea kuzorota kwa hali nchini Ivory Coast na taarifa za karibuni kuhusu mauaji ya halaiki Magharibi mwa nchi hiyo.

Ofisi hiyo imesema inaendelea kukusanya taarifa za madai ya uhalifu unaotekelezwa na pande mbalimbali katika mgogoro huo. Ofisi hiyo imekuwa ikifanya uchunguzi wa awali ivory Coast na hatua itakayofuata itakuwa ni kwa mwendesha mashitaka kutumia uwezo wake ili kuomba idhini ya mahakama kuagiza kufanyika kwa uchunguzi.

Ivory Coast sio mwanachama wa mkataba wa Roma lakini Rais Laurent Gbagbo na Alassane Ouatarra wote wamekubali umuhimu na jukumu la mahakama hiyo. Endapo Mahakam itatoa idhini basi mwendesha mashitaka ataanza uchunguzi na kutayarisha maombi ya vibali vya kukamatwa wanaodaiwa kuhusika na uhalifu nchini Ivory Coast.