Skip to main content

DR Congo yazindua chanjo dhidi ya nimonia kwa msaada wa UM

DR Congo yazindua chanjo dhidi ya nimonia kwa msaada wa UM

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo leo imeongeza chanjo dhidi ya nimonia kwenye mpango wake wa taifa wa chanjo kutokana na mradi maalumu unaofadhiliwa na Umoja wa Mataifa kuhakikisha wanaokoa maisha ya watoto wa chini ya miaka mitano.

Mpango huo unasaidiwa pia na muungano wa kimataifa wa chanjo GAVI ambao unazileta pamoja nchi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la afya duniani WHO na wadau wengine wanaohusika na masuala ya kimataifa ya afya.

Chanjo hiyo itaanza katika majimbo mawili kati ya 11 ili kuzuia ugonjwa huo ambao ni muuaji mkubwa wa watoto wa chini ya miaka mitano Afrika. Mke wa Rais Kabila Bi Olive Lembe Kabila na waziri wa afya wa Congo na wauguzi wa afya wameshuhudia mtoto wa kwanza akipata chanjo hiyo mjini Kinshasa.

Nimonia imeelezwa kuuwa watu zaidi ya milioni moja kila mwaka ikiwa ni pamoja na watoto laki tano wa chini ya umri wa miaka mitano.