Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wabunge wa Somalia wampinga mwakilishi wa UM

Wabunge wa Somalia wampinga mwakilishi wa UM

Takribani wabunge 100 wa serikali ya mpito ya Somalia mwishoni mwa wiki wamefanya mkutano mjini Moghadishu na kumshutumu mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Balozi Augustine Mahiga kuwa anasambaratisha serikali ya mpito.

Wabunge hao wametia saini mswada wa kumpinga balozi Mahiga na kusema watajadili mswada huo kwenye kikao cha kwanza cha bunge.

Wabunge hao wamesema Mahiga anaandaa mkutano ambao wanauona ni kikwazo kwa serikali ya mpito na wanaupinga mkutano huo. Wabunge hao wameiomba serikali ya mpito kugomea mkutano na wamemtaka Balozi Mahiga kuacha kuingilia masuala ya serikali ya mpito.

Ijumaa iliyopita Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa Balozi Mahiga alitoa taarifa kwamba anaandaa mkutano wa ngazi ya juu utakaofanyika Nairobi Kenya April 12 na 13 na kuutaka uongozi wa serikali ya mpito kuhudhuria mkutano huo ambao utajadili masuala mbalimbali ikiwemo mustakhbali wa serikali ya mpito inayotakiwa kumaliza muda wake Agosti mwaka huu.