Elimu kuhusu matatizo ya akili (autism) ni muhimu sana:Ban

Elimu kuhusu matatizo ya akili (autism) ni muhimu sana:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu matatizo ya akili ni muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa kwani mamilioni ya wagonjwa wa akili duniani wanastahili kupewa huduma, kuangaliwa na kuheshimiwa.

Katika ujumbe maalumu kuadhimisha siku hii ambayo kila mwaka hufanyika tarehe pili April amesema matatizo ya akili hayabagui, yanaweza kumpata mtu yoyote na katika nchi yoyote, lakini baadhi ya watu wenye matatizo ya akili au autism wanabaguliwa, kunyanyaswa na kutengwa.

Ameongeza hali hiyo haiwezi kuvumilika kwani ni ukiukaji wa haki za binadamu. Amesema matatizo ya akili ni tatizo gumu, lakini kwa tiba muafaka ya mapema yanasaidia kupunguza makali ya tatizo hilo na ndio maana Umoja wa Mataifa unasisitiza kuelimisha kuhusu dalili za autism na kutoa huduma na tiba ya mapema katika siku za mwanzo za tatizo hilo.

Ban amesema kwa jamii inaweza kusaidia kwa njia nyingi , hasa kwa kuwasaidia wazazi wenye mtoto mwenye matatizo ya akili, kutoa fursa za kazi kwa wenye autism kutokana na ujuzi walionao na pia kwa kuelimisha umma kufikia mahitaji ya elimu ya wanafunzi wenye matatizo hayo kwa kufanya hivyo kila mmoja atafaidika.