Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi zaidi zinahitajika kutekeleza haki za binadamu Paraguay:UM

Juhudi zaidi zinahitajika kutekeleza haki za binadamu Paraguay:UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kidini au imani Heiner Bielefeldt amepongeza mazingira ya uwazi na kuvumiliana nchini Paraguay katika ngazi ya jamii na serikali kwa ujumla.

Bwana Bielefeldt pia amesisitiza katika mwisho wa ziara yake nchini humo kwamba bado kuna fursa ya kuboresha zaidi mipango ya utekelezaji wa haki za binadamu hasa katika masuala ya ubaguzi. Amesema hakuna usawa katika ugawaji wa mali, fursa ya elimu, ushawishi wa kisiasa na katika masuala ya walio wachache. George Njogopa anaripoti.

(RIPOTI YA GEORGE NJOGOPA)

Mtaalamu huyo amebainisha kuwepo kwa mapungufu kadhaa ikiwemo kutokuwepo kwa  taasisi za kidola kwa ajili ya kuhakikisha mbinu za utekelezaji zinazingatiwa. Hali hiyo imedhihiri zaidi katika eneo lijulikana kama Chaco ambako kuna idadi kubwa ya wakazi wanaishi kwenye eneo hilo.

Ametilia wasiwasi wake uwezekano kwa kuwepo kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa haki za binadamu hasa katika eneo la uhuru wa kuabudu kutokana na kukosekana huko kwa mifumo iliyotafsiriwa vyema. Wakazi wa Paraguay wanahistoria ya kukumbana na matukio ya aina mbalimbali ikiwemo unyanyasaji, kutengwa na kunyimwa fursa nzuri za kiuchumi.

Kwenye ziara yake hiyo iliyoanza March 23 hadi 30 mtaalamu huyo amekutana na maafisa wa serikali, pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kiraia na kujadiliana nao masuala mbalimbali.