Ofisi mpya za UNEP na UN-HABITAT zinajali mazingira:UM

31 Machi 2011

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo amezindua ofisi mpya za shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP na shirika la makazi duniani UN-HABITAT mjini Nairobi Kenya.

Ban ameambatana na Rais wa Kenya Mwai Kibaki katika uzinduzi wa ghafla hiyo na amesema nyumba hizo zimejengwa kwa kuzingatia mazingira eneo la Gigiri, na amesema zinakuwa ni mfano bora wa majengo kwenye eneo la Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara.

Ameongeza jengo hilo ni zuri lakini kikubwa zaidi ni mfano wa kuigwa katika kujali mazingira. Amesema ili kizazi kinachozidi kukua hivi sasa kiwe na mustakabali mzuri, basi kunahitajika kuwa usanifu katika ujenzi, kutumia vyema rasilimali, kupunguza uchafu na kuokoa watu na jamii zao.

Sekta ya majengo imeelezwa kuwa mchangiaji mkubwa wa gesi za viwandani duniani huku theluthi moja ya nishati inatumika maofisini na majumbani na ni kutokana na changamoto hizi ndio Umoja wa Mataifa ukaamua kujenga ofisi hizo mpya za UNEP na UN-HABITAT ambazo zinaonyesha ni jinsi gani majengo bora yanaweza kusaidia kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud