Baraza la usalama lafikiria vikwazo zaidi dhidi ya Gbagbo

Baraza la usalama lafikiria vikwazo zaidi dhidi ya Gbagbo

Ufaransa na Nigeria wanasambaza mswada wa azimio kwenye baraza la usalama wakitaka vikwazo zaidi viwekwe dhidi ya Rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast kumshinikiza kuachia madaraka.

Gbagbo amegoma kukabidhi madaraka kwa Alassane Ouattara anayetambulika kimataifa kama mshindi wa uchaguzi wa Rais uliofanyika Novemba mwaka jana. Wakati huohuo mapigano makali yanaendelea nchini Ivory Coast.

Kwa mujibu wa msemaji wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNOCI Hamodon Toure, majeshi yanayomuunga mkono Bwana Ouattara yamechukua udhibiti wa baadhi ya miji iliyokuwa ikishikiliwa na Bwana Gbagbo. Amesema udhibiti huo kwa saa 48 sasa unaendelea kwa utulivu kuliko ilivyotarajiwa.