Miji ni chanzo cha uchafuzi hali ya hewa:UN-HABITAT
Ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la makazi UN-HABITAT inasema miji ndio chanzo kikubwa cha uchaguzi wa hali ya hewa duniani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kimataifa ya UN-HABITAT kuhusu makazi ya watu, miji , mabadiliko ya hali ya hewa na ukuaji wa miji inamaanisha kwamba watu wengi zaidi sasa wanaishi mijini na kwamba wako katika hatari ya kukabiliwa na athari za uchafuzi na mabadiliko ya hali ya hewa. Alice Kariuki ana taarifa kamili.
(RIPOTI YA ALICE KARIUKI)
Ripoti hiyo ilioandaliwa kwa ajili ya mkutano wa Aprili 11 hadi 15 wa nchi wanachama wa baraza linaloangalia mipango ya kazi na bajeti ya UN-HABITAT inasema changamoto kubwa ya mabadiliko ya hali ya hewa iko katika miji.
Mkurugenzi mkuu wa UN-HABITAT Joan Clos amesema miji ni chanzo kikubwa cha gesi ya viwandani, lakini kuna maeneo ambayo mabadiliko yanaweza kufanyika. Ameongeza kuwa uongozi wa miji unaushawishi muhimu kwa masuala ya gesi ya viwandani na kwenda sambamba na mabadiliko ya hali ya hewa.
Hata hivyo ripoti hiyo inasema muda wa kushughulikia changamoto hizo ni sasa, miji iliyopangika vizuri, yenye mfumo bora wa usafiri na mikakati imara inaweza kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa.